UJUMBE WA BABA MTAKATIFU KUHUSU SIKU YA MISIONI DUNIANI TAREHE 22 OKTOBA, 2006 DHAMIRA: “Upendo, Kiini cha Umisionari” Wapendwa kaka na dada zangu, 1. Siku kuu ya Umisionari Duniani tunayoadhimisha leo tarehe 22 Oktoba, inatupatia nafasi ya pekee ili kutafakari kuhusu mada: “UPENDO, KIINI CHA UMISIONARI” Umisionari kama usipotegemezwa na Upendo, usipotokana, yaani na Upendo wa Ki-Mungu, unariski kujishusha na kuwa kama huduma tu ya kijamii. Upendo ambao Mungu anatoa kwa kila mmoja unaunda roho ya uzoefu na uenezaji wa Injili, kwa wale waipokeao wanakuwa ndio mashahidi. Upendo wa Mungu ambao ni uhai kwa ulimwengu ni Upendo tuliopewa katika Yesu, Neno la Wokovu, sura wazi ya huruma ya Baba wa mbinguni. Ujumbe wa Wokovu unaweza kufupishwa kwa hiyo kwa kutumia maneno ya Mwinjili Yohane. “Kwa hilo upendo wa Mungu umejidhihirisha. Mungu amemtuma mwanae wa pekee duniani, ili sisi tupate uzima katika yeye.” [1 Yh. 4:9] Utume wa kueneza ujumbe wa Upendo huu, Yesu aliutoa kwa Mitume baada ya ufufuko wake, na Mitume wakiwa wamebadilishwa ndani mwao na Roho Mtakatifu katika siku ya Pentekoste, wakaanza kutoa ushuhuda wa Bwana wao aliyekufa na kufufuka. Kutoka hapo, Kanisa linaendeleza utume huo huo wa Kimisionari ambao unatangaza kwa waamini wote wajibu wa daima bila kurudi nyuma. 2. Kwa hiyo kila jumuiya ya Kikristo inaalikwa kutangaza kuwa Mungu ni Upendo. Ni katika fumbo hili muhimu la imani yetu nimependa kutafakari katika Ensiklika “DEUS CARITAS EST” (Mungu ni upendo). Katika upendo wake, Mungu anatoa zawadi kwa vizazi vyote katika historia ya binadamu. Hapo mwanzo mwanadamu alikuja kutoka mikononi mwa Muumba kama tunda la Upendo. Dhambi ikatia kiza katika mwanadamu,ambaye ni mhuri wa ki-Mungu. Walipodanganywa na yule mwovu, mababu zetu Adamu na Eva, walipoteza ule uhusiano mzuri wa kuaminika kati yao na Mungu, wakaamini kile kishawishi cha yule mwovu aliyeamsha ndani yao ile roho ya ujuvi (udadisi) ya kwamba Mungu yu na wivu kama binadamu hivi ana lengo la makusudi la kuwanyima uhuru wao. Hivyo wao walichagua kufuata uhuru wao ulio na mipaka badala ya kufuata Upendo wa bure kutoka kwa Mungu. Hatimaye kama matokeo waliishia kupoteza furaha ya dhati na hivyo kuonja uchungu wa mateso ya dhambi na mauti. Lakini Mungu hakuwatupa, bali aliwaahidia wao na vizazi vyao wokovu, akaahidi kumtuma Mwanae wa pekee, Yesu, ambaye angefunulia wazi kuhusu ukamilifu wa nyakati, Upendo wake wa Kibaba, Upendo wenye uwezo wa kumwondoa kila mwanadamu kutoka utumwa wa dhambi na mauti. Hivyo kwa njia ya Kristo tumepokea uzima wa milele, uzima ule ule katika Utatu Mtakatifu. Shukrani kwa Kristo mchungaji mwema ambaye hawaachi kondoo wapotee. Wanadamu wa nyakati zote wamepewa uwezekano wa kumrudia Mungu Baba mwenye upendo, aliye tayari kumpokea mwana mpotevu. Ishara ya Upendo kama huo usio na mipaka ni Msalaba. Katika kifo cha Msalaba cha Kristo, nimeandika katika Ensiklika.“DEUS CARITAS EST” (Mungu ni Upendo), hapa kinafanyika kitendo cha Mungu kujitoa mwenyewe ili kumwinua mwanadamu na kumkomboa kwa Upendo, upendo ule wa dhati kabisa. Ni kwa njia hiyo ukweli huu unakamilika. Na kutoka hapo ndipo inajieleza wazi upendo ni kitu gani. Kutokana na muono huu mkristo anapata njia ya kuishi uhai wake, katika Upendo. (Na. 12) 3. Katika vijilia ya mateso yake, Yesu aliwaachia wosia wanafuzi wake waliokuwa katika karamu ya mwisho ili kuadhimisha Pasaka, “Amri mpya ya mapendo MANDATUM NOVUM”. (“Amri mpya nawapeni, Pendaneni” Yoh. 15:17). Upendo wa kidugu ambao Yesu anawatakia “maraki” zake, asili yake ni katika Upendo wa Kibaba wa Mungu. Kama anavyobaini mtume Yohane: “Anayependa ametoka kwa Mungu, na anamjua Mungu” (1Yh. 4:7). Kwa hiyo ili kupenda kama Mungu ni budi kuishi ndani yake na katika yeye: Makazi ya kwanza ya mwnadamu ni Mungu na ni yeye yule aishie katika yeye tu ana ule moto wa Upendo wa Mungu wenye uwezo wa “kuutia nuru” ulimwengu. Hii ndiyo kazi ya Kanisa katika nyakati zote. Hapa si vigumu kuelewa kuwa hamasa mahususi ya kimisionari, kazi muhimu ya kwanza ya jumuiya ya kanisa, ni uaminifu katika Upendo wa mungu, na hii ni kwa kila mkristo na kwa kila jumuiya mahalia na katika kila kanisa mahalia kwa watu wote duniani. Ni katika kuelewa juu ya wajibu huu wa Kimisionari katika jumuiya, ambapo jumuiya ya mitume wa Yesu inachota ule utayari wa upendo katika kufanikisha kazi ya kuendeleza maisha ya kiutu na kiroho katika ushuhuda, kama alivyoandika mpendwa Yohane Paulo II katika Enjiclika “REDEMPTORIS MISSIO, “KIINI CHA SHUGHULI NZIMA YA Kimisionari ni Upendo ambao ndio unaendeleza umisionari na ambao ni kipimo pekee ambapo ni kwayo tu yote yapaswa kutendeka au kutotendeka, kubadilishwa au kutobadilishwa. Ndicho kiini kinachopaswa kuongoza kila tendo na ambacho yote yapaswa kuelekea. Iwapo yote yatafanywa kwa kufuata dira ya Upendo au kwa kuongozwa na Pendo hakuna lisiloweza kupendeza na yote huwa mema”. (Na. 60). Kwa hiyo kuwa mmisionari maana yake ni kumpenda Mungu kwa dhati hadi hata kumtolea uhai. Ni mapadre, watawa na walei wangapi hata katika nyakati zetu hizi wametoa ushuhuda wa upendo kwa njia ya kifo kama mashahidi. Kuwa mmisionari maana yake kunyenyekea (kujishusha) kama msamaria mwema mbele ya shida za wengine, hasa za walio maskini na wahitaji, kwa sababu aliye na upendo katika Kristo hatafuti faida yake mwenyewe, bali ufalme wa Baba na kwa faida ya jirani. Hii ndiyo siri ya mafanikio ya kazi ya utume wa kimisionari hadi kuvuka mipaka na tamaduni ili kuwafikia mataifa na kuenea hadi miisho ya dunia. 4. Wapendwa kaka na dada zangu, siku ya Usimionari Duniani iwe wakati mwafaka wa kuelewa vizuri zaidi kuwa ni ushuhuda wa upendo, ambao ni kiini cha Umisionari unaomhusu kila mmoja. Kuitangaza Injili ieleweke kuwa si kazi ya mtu binafsi, bali ni kazi ya pamoja, ya kila jumuiya. Tunakuwa karibu na wale walio mstari wa mbele katika uinjilishaji na hapa nawafikiria na kuwatambua wamisionari wa kiume na wakike, na wengi wengineo, watoto, vijana, watu wazima ambao kwa njia ya sala na ushirkiano wao kwa njia mbali mbali wanachangia kazi ya kuendeleza ufalme wa Mungu duniani. Ni mategemeo yangu kwamba ushirikiano huu ukue na utadumu daima kwa wote. Natumia nafasi hii kupongeza kazi kubwa ya tume, ya Uinjilishaji wa watu wote na ya mashirika ya Kipapa ya Kimisionari (PMS) ambayo kwa juhudi kubwa yanasimamia na kuunganisha juhudi za walio mstari wa mbele pande zote duniani katika umisonari. Bikira Maria ambaye kwa uwepo wake pale msalabani na kwa sala zake katika karamu ya mwisho alishiriki katika juhudi za mwanzo wa kazi za umisionari katika kanisa, asimamie kazi zao na awasaidie waamini katika Kristo ili wawe daima na Upendo wa kweli, ili katika ulimwengu huu wenye kiu kabisa ya kiroho wawe chemchemi ya maji ya uzima. Nawatakia hayo kwa moyo wangu wote, nawabariki nyote. Kutoka Vatikano, 29 Aprili, 2006 [Sahihi], (BENEDICTO XVI) PAPA 3 3