UJUMBE WA BABA MTAKATIFU KWA AJILI YA DOMINIKA YA ULIMWENGU YA MISIONI 2001 Misericordias Domini in aeternum cantabo (Ps 89 [88]: 2 Fadhili za bwana nitaziimba milele (Zb 89 [88]:2) Wapendwa Kaka na Dada, 1. Kwa furaha ya ndani kabisa tuliadhimisha Yubilei Kuu ya wokovu, nyakati za neema kwa Kanisa lote. Huruma ya Mungu, ambayo kila mwamini aliguswa nayo, inatusukuma. "Kutweka mpaka kilindini." Tukikumbuka kwa shukrani zama zilizopita, tukiliishi kwa shauku zama hizi na tukitazamia kwa matumaini zama zijazo, tukiamini kwamba "Yesu Kristo ni yule yule, jana leo na hata milele" (Ebr 13:8) -- (rej. barua ya kitume Novo Millenio Ineunte, n.1). Huko kuelekea zama zijazo, tukiangaziwa na tumaini, sharti uwe ni msingi kwa ajili ya utendaji wote wa kanisa katika milenia mpya. Huu ndio ujumbe ninaotamani kumletea kila mkatoliki kwa nafasi ya Dominika ya Misioni, ambayo itaadhimishwa tarehe 21 Oktoba. 2. Kwa hakika, ni wakati muafaka wa kuangalia mbele, tukiukazia macho yetu uso wa Yesu (rej. Ebr 12:2). Roho anatuita "kuelekeza mawazo yetu kwa zama zijazo zilizo mbele yetu"(Novo Milenio Ineunte, n.3), kumshuhudia na kumtangaza Kristo, tukimshukuru "kwa ajili ya maajabu ya Bwana aliyotutendea" Misericordias Domini in aeternum cantabo [Fadhili za Bwana nitaziimba milele (Zab 89:1). Katika nafasi ya Dominika ya Misioni mwaka uliopita, niliwakumbusheni kwamba sharti la umisionari lazaliwa na tafakari motomoto ya Yesu Mkristo ambaye amemtafakari Yesu Kristo hawezi kushindwa kuakiswa na mionzi yake (rej. Maisha ya Wakfu, n.14) na kujifunga mwenyewe kutoa ushuhuda wa imani yake katika Kristo, mwokozi pekee wa wanadamu. Tafakari ya uso wa Yesu yapelekea wafuasi kutafakari nyuso za wanaume na wanawake wa leo. Bwana anajifananisha kwa yamkini na hao ndugu zangu walio wadogo" (rej. Mt 25: 40, 45). Tafakari ya Yesu mwinjilishaji namba moja na mkuu kabisa" (Evangelii Nuntiandi, n.7) yatugeuza kuwa wainjilishaji. Yatufanya tutambue tamaa yake ya kutoa uzima wa milele kwa wale waliokabidhiwa kwake na baba (rej.Yn 17:2.). Mungu hutaka watu wote waokolewe, na kupata kujua yaliyo kweli' (1 Tim 2:4) na Yesu alijua kwamba mapenzi ya baba kwake yalikuwa kwamba alitakiwa kutangaza ufalme wa Mungu katika miji mingine: "Maana kwa sababu hiyo nalitumwa"(Lk 4:43). Matokeo ya kuwatafakari "hao ndugu zake walio wadogo" ni ufumbuzi kwamba kila mtu, ingawa kwa namna ambayo kwetu ni fumbo, anamtafuta Mungu ambaye ameumbwa naye na anapendwa naye. Wafuasi wake wa kwanza waligundua hilo: "[Bwana] wote wanakutafuta' (Lk 1:37). Nao "Wayunani" kwa niaba ya vizazi vijavyo, wanaguta kwa hamu: sisi tunataka kumwona Yesu" (Yn 12:21). Ndiyo, Kristo ndiye nuru kweli inayomwangazia kila mtu anayekuja ulimwenguni (rej.Yn 1:9): "mwanadamu anamtafuta kwa kupapasa " (Mdo17:27) akivutwa na mvuto wa ndani ambao chanzo chake hata wao. Kimefichika katika moyo wa Mungu, pale inapopigapiga hamu kwa ajili ya wokovu wa wote. Mungu anatufanya sisi mashahidi na wapiga mbiu wake. Kwa lengo hilo anatujaza, kama katika pentekoste mpya, moto wa Roho wake, upendo wake na uwepo wake. "Nipo pamoja nanyi, hata ukamilifu wa dahari" (Mt 28:20). 3. Tunda jingine la Yubilei kuu ni ile hali ambayo Bwana anamtaka kila Mkristo kutazama mbele kwa imani na matumaini. Bwana antupa heshima ya kuweka matumaini yake juu yetu na kutuita kwa ajili ya huduma hiyo na kutuonyesha huruma yake (rej. Tim 1:12,13). Mvuto haupo kwa ajili ya wachache tu, bali ni kwa kila mmoja kadiri ya hali yake ya maisha. Katika barua ya kitume Nuovo Millenio Ineunte niliandika kuhusu neno hilo: Shauku hii haitashindwa kuchochea katika kanisa hisia mpya za utume, ambao hauwezi kuachiwa kwa kundi la "wataalamu" tu, bali utataka uwajibikaji wa wanajumuiya wote la taifa la Mungu Wale waliofikia uhusiano halisi wa Kristo hawawezi kumhifadhi kwa ajili yao tu, bali hawana budi kumtangaza. Mtazamo mpya wa utume unahitajika, ambao wataishi kama sharti la kila siku la jumuiya za Kikristo na vikundi. Kristo lazima awekwe mbele ya watu wote kwa matumaini. Tutawahubiria watu wazima, familia, watoto, bila hata kuficha madai yaliyo ya msingi sana ya ujumbe wa injili. Lakini tutafanya hivi kwa kuzingatia mahitaji ya kila mmoja kadiri ya hisia zao, lugha, mithili ya Paulo aliiyetamka, "Nimekuwa hali zote kwa watu wote, ili kwa njia zote nipate kuwaokoa watu" (1Kor 9:22) (n.40). Wito kwa ajili ya utume unapata umuhimu wa peke yake hasa kama tunaangalia sehemu ile ya watu ambayo bado haimjui Kristo au haimtambui. Ndiyo kaka na dada, utume kwa "mataifa" [ad gentes] leo ni halali zaidi na zaidi kuliko wakati mwingine wowote. Ninavutiwa moyoni mwangu na nyuso za watu ambao nimeweza kuwatafakari wakati wa hija zangu: uso wa Kristo unaoakisiwa katika ule uso wa maskini na wateswa: uso wa Kristo unaoakisiwa katika wale wanaoishi kama kondoo wasio na mchungaji"(Mk 6:34). Kila mwanamume na mwanamke ana haki kufundishwa "mambo mengi" (Mk 6:34). Alikabiliwa na ukweli wa udhaifu wa kibinadamu na kutojitosheleza, kishawishi cha kibinadamu, na kwa mtume kadhalika, ni kuwaaga watu waende zao. Lakini badala yake ni wakati huuhuu kwamba, kutafakari uso wa mpendwa, kila mmoja wetu hana budi kusikiliza tena maneno ya Yesu: "hawana haja ya kwenda zao". "Wapeni ninyi chakula" (rej. Mt 14:16; Mk 6:37). Kwa namna hiyo tutang'amua papo hapo udhaifu wa kibinadamu na neema ya Bwana. Tukitambua udhaifu wa kibinadamu usiokwepeka unaotutia alama kwa undani kabisa, tunahisi lazima ya kumtolea Mungu shukrani kwa kile alichotenda ndani yetu na kwa kile chote ambacho bado atafanya kwa neema yake. 4. Tutashindwaje, kuwakumbuka katika mazingira haya, wamisionari wote, mapadre, watawa na walei walioufanya utume kwa mataifa (ad gentes) na kwa uzima (ad vitam) uwe sababu yao ya kuishi? "Kwa maisha yao wanatangaza neema za Bwana bila mwisho" (26:89). Si mara chache "bila mwisho huo" imefikia hatua ya kumwaga damu. Jinsi gani walivyo wengi "mashahidi wa imani" karne hii ya mwisho!" Ni kwa sababu ya kujitoa kwao kwa ukarimu ufalme wa Mungu uliweza kukua. Kumbukumbu zetu ziwaendee hao, zikiambatana na sala zetu. Mfano wao unatoa kichocheo na tegemeo kwa waamini wote ambao wanaweza kujipa moyo wanapojiona "wanazungukwa na wingu kubwa la mashahidi namna hii" (Ebr 12:1), ambao kwa matendo na maneno yao wameifanya na wanaendelea kuifanya Injili ivume katika kila bara. Ndiyo, kaka na dada, hatuwezi kukaa kimya juu ya yale tuliyoyaona na kusikia (rej. Mdo 4:20). Tumeiona kazi ya Roho na utukufu wa Mungu ukijionyesha katika udhaifu (rej. 2Kor 12; 1 Kor 1). Vivyo hivyo hata leo wanaume wengi na wanawake wengi, kwa majitoleo yao na sadaka zao, ni udhihirisho hai wa upendo wa Mungu. Kutoka kwao tunapata imani, nasi kwa zamu yetu, tunahimizwa kuwa watangazaji na mashahidi wa Fumbo. 5. Utume ni tangazo la furaha la zawadi iliyo kwa ajili ya wote, na ambayo ni ya kutolewa kwa watu wote kwa heshima kubwa kabisa kwa ajili ya uhuru wa kila mmoja: zawadi ya ufunuo wa Mungu ambaye ni upendo, Mungu ambaye "aliupenda hivi ulimwengu hata akamtoa mwanae wa pekee "(Yn 3:16)...kwa hiyo kanisa haliwezi kuacha utendaji wake wa kimisionari kati ya watu na ulimwengu. Ndiyo shughuli yake ya kwanza ya utume kwa mataifa (ad gentes) kutangaza kwamba ni katika Kristo "Njia, na kweli, na Uzima"(Yn 14:6) watu wanapata wokovu (Novo Millenio Ineunte, n.50). Huu ni mwaliko kwa wote, ni wito wa haraka unaostahili jibu karimu na la papo hapo kama Maria mama wa Yesu; kama wachungaji baada ya kushtushwa na tangazo la Malaika; kama Maria Magdalena mbele ya Kristo mfufuka. "Mwanzoni mwa karne hii mpya, hatua zetu lazima ziharakishe kadiri tunavyotembea juu ya barabara kuu za ulimwengu Kristo mfufuka anatutaka tukutane naye kama vile ilivyokuwa mara moja katika chumba ghorofani, jioni ya "siku ya kwanza ya juma"(Yn 20:19). Alipowatokea wafuasi wake ili "kuwavuvia"Roho wake atiaye uzima na kuanzisha ndani yao utajiri mkubwa wa kutangaza Injili (Novo Millenio Ineunte, n.58) 6. Wapendwa kaka na dada! Utume unataka sala na kujitosa kwa vitendo. Mahitaji ni mengi kwa ajili ya mweneo kama wa mishipa ya damu wa Injili Mwaka huu ni wa 75 tangu ianzishwe Dominika ya Misioni na Papa Pio XI, ambaye alipokea ombi la kila Chama cha Kipapa kwa ajili ya kueneza Imani,"kuanzisha" siku ya sala na propaganda kwa ajili ya misioni." "Inayopasa kuadhimishwa siku hiyohiyo moja katika kila jimbo, parokia na taasisi za ulimwengu Katoliki na kuhimiza matoleo kwa ajili ya misioni " ( Idara Takatifu ya Madhehebu: Uanzishaji wa Dominika ya Misioni,14 Aprili 1926 AAS 19 (1927), n.23nn). Tangu hapo Dominika ya Misioni imekuwa ni nafasi ya pekee kuwakumbusha Taifa lote la Mungu juu ya uhalali wa kudumu wa amri ya umisionari kwani kazi ya kimisionari ni suala la Wakristo wote, la majimbo yote na parokia zote, taasisi za Kanisa na Vyama" (Waraka wa Baba Mtakatifu. Utume wa mkombozi Redemptoris Missio, n.2). Papo hapo ni nafasi ya kufaa kuthibitisha tena kwamba "misioni haziombi michango tu, bali zinaomba kushirikishana katika kazi ya kuhubiri na kusaidia wenye shida. "Kila kitu tulichopata kutoka kwa Mungu, uhai wenyewe na mali si mali yetu" (n.81). Siku hii ni ya maana katika maisha ya kanisa "kwa sababu inafundisha jinsi ya kutoa kama toleo linalofanywa kwa Mungu katika adhimisho fulani la Ekaristi na kwa ajili ya Misioni za ulimwengu (n.81). Siku hii ya kukumbuka kuanzishwa Dominika ya Misioni iwe ni nafasi muafaka kutafakari juu ya hitaji kubwa zaidi na la pamoja la kuendeleza Roho ya Kimisionari na kukusanya misaada ya lazima na vitu ambavyo wamisionari wanavihitaji. 7. Katika homilia kwa ajili ya kufunga Yubilei kuu, tarehe 6 Januari 2001 nilisema: "Yatupasa kuanza upya toka kwa Kristo kwa ari ya Pentekoste, kwa shauku mpya. Kuanza toka kwake zaidi ya yote aliye juu katika kujitosa kwetu kwa kila siku, katika utakatifu, kwa mwelekeo wa sala na kusikiliza neno lake. Kuanza kutoka kwake ili kushuhudia upendo wake" (n.8). Kwa hiyo: Anzeni upya kutoka kwa Kristo, ninyi mliopata huruma. Anzeni upya kutoka kwa Kristo, ninyi mliosamehe na mliosamehewa. Anzeni upya toka kwa Kristo, ninyi mnaojaribiwa na uvuguvugu:mwaka wa neema hauna mwisho. Anzeni upya toka kwa Kristo, Kanisa la millenia mpya. Imbeni kadiri mnavyoenda (rej. Ibada ya kufunga Misa ya Epifania ya Bwana 2001). Maria, mama wa kanisa, Nyota ya Uinjilishaji, utusindikize katika safari yetu kama alivyobaki pamoja na wafuasi siku ile ya Pentekoste. Kwake tunaenda kwa matumaini. Kwa njia ya maombezi yake, Bwana atujalie paji la udumifu katika wajibu wetu wa kimisionari ambao ni suala la jumuiya nzima ya Kanisa. Kwa hisia hizo za moyoni ninawabariki. Toka Vatikano, Juni 2001, Sherehe ya Pentekoste.